UMUHIMU WA UMOJA KWENYE FAMILIA - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Tuesday, July 17, 2018

UMUHIMU WA UMOJA KWENYE FAMILIA


Jana tuliangalia sababu za migogoro kwenye familia na tuliona ni sababu kuu tano japo zilielezewa kwa kifupi sana leo tunaingia kipengele kingine cha umoja katika familia

Kama upo kwenye ndoa na bado hujaelewa haya mahesabu basi ni vema ukajifunza sasa 1+1=1 kwenye familia na siyo 2 yaani mtu akikichukua wewe akajumlisha na mmeo jibu ni moja

Unaweza kuthibitisha hili kimaandiko Mwanzo 2:24 "Kwa hiyo Mwanamume atamuacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja"

Neno hilo halijasema watakuwa miili miwili tofauti bali watakuwa mwili mmoja yaani mnakuwa kitu kimoja, hivyo mtu akimwona mmeo kakuona wewe

Kama hukusoma makala ya jana ya Kwa nini kuna migogoro kwenye familia ⇒⇒⇒UNAWEZA KUGUSA HAPA KUISOMA

Lakini kingine kinachoonekana hapo ni kwamba mnaachana na wazazi wenu maana yake ni kwamba mkeo/mumeo anachukua nafasi ya pili katika maisha yenu ambayo nafasi hii ilikuwa inachukuliwa awali na wazazi wako

Nafasi ya kwanza inajulikana ni ya Mungu hivyo wazazi wanakuwa nafasi ya tatu baada ya kuoa au kuolewa hii haimaanishi usiwaheshimu au uwadharau hapana ila kimaandiko inapaswa kuwa hivyo na hauwezi kutengua neno la Mungu

Miili yetu ina viungo mbalimbali ambavyo vikifanya kazi kwa pamoja ndio vinasababisha sisi kuwa binadamu aliyekamilika na mwenye maana Waef 4:16 "Katika yeye mwili wote ukiungamanishwa na kushikanishwa kwa msaada wa kila kiungo, kwa kadiri ya utendaji wa kila sehemu moja moja, huukuza mwili upate kujijenga wenyewe katika upendo.

Kadhalika na kwenye ndoa tupo na miili tofauti lakini tu wamoja kila mtu ana majukumu yake anayopaswa kuyafanya ili ndoa ipate kusimama na kuwa na upendo na amani wakati wote

Mwanamume ni lazima asimame katika majukumu yake ya kuitunza familia na mwanamke ni lazima asimame katika majukumu yake ya kuilea familia Warumi 12:4
"Kwa kuwa kama vile katika mwili mmoja tuna viungo vingi, wala viungo vyote havitendi kazi moja;

Waefeso 4:3 "Na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani, hivyo ni muhimu sana kuwa na umoja katika familia umoja ndio unaoleta amani ya kudumu katika familia

Katika familia hamuwezi kumuona Mungu kama hamtadumisha kupendana na pendo lake kuwa katikati yenu 1Yoh 4:12 "Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote. Tukipendana, Mungu hukaa ndani yetu, na pendo lake limekamilika ndani yetu.

Mnapoweza kuwa na upendo katikati yenu mnaweza kunena mamoja, kwa sababu katika familia haipaswi mmoja kusema hivi na mwingine vile bali wote mnanuia na kunena kimoja na Mungu hukibariki

1Kor 1:10 "Basi ndugu, nawasihi, kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba nyote mnene mamoja; wala pasiwe kwenu faraka, bali mhitimu katika nia moja na shauri moja.

Siku ambayo mnayoanza kufichana mambo ndio Shetani anaanza kujizolea utukufu kwenye ndoa kwa kuwa si wawili tena mmekuwa wamoja hakuna kuficha kitu chochote iwe ni biashara, mshahara au jambo lolote lile

Na kumdanganya mke au mme wako ni kujidanganya wewe je unaweza kudanganya sehemu ya mfupa wako? Huoni unajidanganya peke yako huoni unajiumiza peke yako?

Kwenye familia ni heri ukweli unaouma kuliko uwongo uliofichwa ambao ukigundulika na mmoja huzaa sumu isiyoweza kumalizika kwa dawa na ndio maana hakuna neno changu kwenye ndoa bali kuna vyetu

SEHEMU YA MSAMAHA:

Japokuwa katika ndoa mnakuwa mwili mmoja katika Kristo Yesu ila ni lazima mthamini tofauti baina yenu wenyewe, malezi na makuzi yapo tofauti kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine

Unachokithamini wewe kinaweza kuwa siyo cha thamani kabisa kwa mwenzio na ndio maana Wanaume walihusiwa sana kuishi na wake zao kwa akili

Kukosea au kwenda kinyume na makubaliano ni jambo la kawaida na pale mtu anapokosea hana budi kusamehewa maana usipomsamehe mwenzako unajitengenezea uchungu ndani yako

Wakolosai 3:13 "mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi.

Hivyo kuna mambo ya kubebeana katika familia, hakuna sababu ya kukaa na kuanza kumlaumu mwenzako na kumuona hafai kwa sababu katenda jambo fulani bali unamsamehe 

Kama unatamani kujiunga na mtandao wa Wanawake wa kujifunza neno la Mungu na kusimama ili uweze kulijua kusudi lako bado unakaribishwa unaweza kuwasiliana nasi kwa whatsup namba 0715113636

Mwanamke Thamani "Wewe umewazidi wote"

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana