JE UNAJUA UPEPO HAUAMUI UELEKEO WA MELI? - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Thursday, February 8, 2018

JE UNAJUA UPEPO HAUAMUI UELEKEO WA MELI?

Meli  moja inakwenda mashariki nyingine wakati huo huo inakwenda magharibi kwa upepo ule ule unaovuma

Mtu mwingine anafurahia na kushukuru ukuu wa Mungu kwenye maisha yake, mwingine analaumu na kulaani kila hatua anayoipitia

Mmoja anafurahia misimamo na misingi imara aliyojiwekea tokea awali ambayo sasa hivi inampatia baraka, furaha na mafanikio imara mwingine anabadili misimamo yake kwa kuangalia yanayoendelea

Kama hukusoma makala ya jana ya Kwa nini ni kubwa kuliko nini unaweza KUBOFYA HAPA

Wapo watu wengi waliobadili misimamo yao baada tuu ya kushawishiwa na vitu  fulani na kusahau kabisa ahadi za Mungu maishani mwao mtizame Gehazi 2Wafalme 5:19--" Lakini Gehazi, mtumishi wa Elisha mtu wa Mungu, akasema, Tazama, bwana wangu amemwachilia huyo Naamani Mshami, asivipokee mikononi mwake vile vitu alivyovileta; kama BWANA aishivyo, mimi nitamfuata mbio, nipokee kitu kwake

Baada ya hapa kwa sababu aliruhusu kutawaliwa kwa fikra zake kwa tamaa ukoma wa Naaman ulihamia kwake na kizazi chake

Usiruhusu changamoto unazopitia kwa muda fulani zitawale maamuzi na misimamo uliyojiwekea juu ya vitu fulani

Wapo watu wengi wanapitia changamoto kidogo tuu wanabadili misimamo yao kabisa, kanisani hawataki kwenda, wanakuwa watu wa kulaumu kila mtu yaani wanabadilika kabisa

Hivi unajua ukikosa fedha ya kula au nauli maana yake ni ufunge, utembee kwa miguu au ufanye kazi zaidi lakini siyo sababu ya kubadili msimamo wako au kwenda kuomba au kuiba?

Msingi wa maisha yetu ni misimamo tunayojiwekea ukikosa msimamo hauna tofauti na mtu asiyekuwa na Imani, Imani inaamua msimamo alionao mtu, msimamo unaamua matendo, hivyo wakati mwingine Imani=msimamo=matendo, Yakobo 2:18 " Lakini mtu atasema, Wewe unayo imani, nami ninayo matendo. Nionyeshe imani yako pasipo matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu

Ni imani ya Danieli kwa Mungu ilimfanya awe na msimamo na kumtamkia Mfalme Nebukadreza maneno haya Daniel 3:18 " Bali kama siyo hivyo,ujue, sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala kuisujudia iyo sanamu uliyoianzisha, ni Imani hiyo hiyo ilimfanya Yoshua mwana wa Nuni kuwa na msimamo wa atakayemtumikia Yoshua 24:14-15 "Nanyi kama mkiona ni vibaya kumtumikia Bwana, chagueni leo mtakaemtumikia.......,lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia Bwana.

Ukikosa Imani unafananishwa na wimbi la bahari Yakobo 1:6 "Ila na aombe kwa imani, pasipo shaka yo yote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku"

Mabinti wa Mwanza na kina Mama tarehe 8-10 nitakuwepo Buzuruga EAGT Kanisani kuzungumza na nyie usitamani kukosa hata kidogo taarifa zaidi tizama tangazo hili hapa    ↧↧↧↧↧↧

Mazingira yale yale na nchi ile ile kuna watu wanaolalama maisha magumu, vyuma vimekaza, Serikali haiwajali lakini pia kuna watu wanaoshinda wakimshukuru Mungu kwa mipenyo wanayoipata katika biashara, kazi na mipango yao

Watu wa agano husitawi na kufanikiwa wakati wengine wanalalama ndio maana Yusufu alikuwa tajiri wakati Israeli kuna njaa, wakati kuna njaa ndipo yule mama mjane analipa madeni yake baada ya kutii mtumishi wa Mungu Elisha

Siyo upepo unaamua meli ielekee wapi bali ni ueleleo ambao nahodha  anataka meli iende, siyo hali ya uchumi na maneno watu wanayoyasema yanaamua upate nini maishani mwako bali ni imani yako kwa Mungu, msimamo pamoja  na matendo yako

Siyo changamoto wala matatizo yanaamua tufanye jambo hili na tuache lile bali ni namna ambavyo tunavyokuwa tumeziweka fikra na akili zetu zote kwa Mungu kutuongoza katika kila maamuzi tunayoyafanya 

Kilichopo nyuma yetu, karibu yetu, mbele yetu au pembeni yetu ni kidogo sana ukilinganisha na kilichopo ndani yetu, tumeumbwa kwa namna ya kipekee na ajabu na tukimtegemea Mungu anatuwezesha kufanya mambo makubwa na ya ajabu

Mtu akigundua kitu kipya hamshangazi Mungu ila anamfurahisha kwa sababu hakuna jambo jipya hata moja chini ya dunia yote yalishakuwepo tangia awali, sema mtu wa kuyaleta kutokea stoo ndio alikuwa hajatokea

Mhubiri 1:10 "Je! Kuna jambo lo lote ambalo watu husema juu yake, Tazama, ni jambo jipya? Limekwisha kuwako, tangu zamani za kale zilizokuwa kabla yetu sisi

Haitoshi Nabii Suleiman akasema "Awazavyo mtu nafsini mwake ndivyo alivyo" hakuna mtu aliyebora zaidi ya fikra zake (you are not better than your thoughts)

Ukifikiri unaweza kwa sababu aliyeko ndani yako ni mkuu utaweza, ukifikiri kidogo utapata kidogo, ukitafuta sababu za kushindwa badala ya kushinda utazipata, ukifikiri huwezi hutokaa uweze, ukifikiri una nguvu na akili ya kufanya utaweza kufanya

Nilichojifunza na nachoendelea kukiona katika maisha ni hiki
hakuna jambo lolote gumu lisilokuwa na ufumbuzi kama kweli  tukimtegemea Mungu na kutumia jitihada zetu zote katika kulitafutia ufumbuzi

Mwanamke Thamani "Wewe umewazidi wote"

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana