NGUVU YA MSAMAHA-III - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Tuesday, January 9, 2018

NGUVU YA MSAMAHA-III



Tumeshajifunza kwamba ni vigumu sana watu ambao mmelelewa mazingira tofauti kukaa pamoja bila kukoseana, ni lazima mtakoseana kwa sababu ya utofauti wenu

Lakini tofauti baina yetu zipo kwa ajili ya kutujenga na kutuimarisha na siyo kutubomoa au kutuharibu ndiyo maana tunapaswa kufurahia utafauti wetu, kama jana haukusoma sehemu ya pili ya Nguvu ya msamaha Gusa hapa kuisoma

Kila mmoja ni imara sana katika eneo fulani na dhaifu katika eneo jingine, hali hii inaleta uhitaji wa mtu mwingine katika eneo lenye udhaifu

Ukiangalia kwa takwimu ugomvi na mfarakano kwenye ndoa kichocheo cha kwanza ni fedha na cha pili ni kukosekana kwa moyo wa msamaha kati ya wanandoa

Mara nyingi watu wamekuwa wanaingia katika mtego wa Shetani wa kumtamkia tuu mtu mdomoni nimekusamehe lakini ndani ya mioyo yao wana vidonda na wanabubujika machozi

Hivyo utakuta mtu akimkosea mwenzake anamuhesabia makosa anapokuja kumkosea tena anamwambia unakumbuka siku fulani ulinifanyia abcd.....

Tayari kwa kufanya hivyo moyo wake unajawa na hasira, chuki na huzuni kwa sababu hata mara ya kwanza hakuwa amesamehe kama alivyosema

Kusamehe haimaanishi kwamba unaigiza  kama vile hukuwahi kukosewa bali ni unaachilia kile ulichokosewa kutokea ndani ya moyo wako 

Kusamehe siyo jambo la akili bali ni suala la moyo na hii ndiyo maana inakuwa ni suala gumu na lenye kuhitaji upendo wa kimungu ambao upo mioyoni mwetu

Tunawezaje kusamehe?

Unapaswa kukumbuka kwamba wale ambao wamekukosea ni binadamu kama wewe na hakuna aliyemkamilifu, pengine hawakupenda kukukosea na pia hawajakamilika kuna siku na wewe utakosea na utahitaji msamaha kama wao

Yakobo 1:2 "Maana twajikwaa sisi sote katika mambo mengi, mtu asiyejikwaa katika kunena huyo ni mkamilifu....."

Unapaswa pia kufahamu kipindi unasamehe mtu aliyekukosea haufanyi dhambi bali unatimiza neno la Mungu, Mathayo 6:14-15 "Kwa maana mkiwasamehe  watu makosa yao na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi, bali msipowasamehe nanyi hamtosamehewa"

Tambua baraka ambazo utazipata kwa kusamehe, unapokuwa na kinyongo inakuwa ni vigumu kukuwa kiimani (spiritual growth) lakini unapoondoa kinyongo kunakufanya kutulia, utaimarika afya yako na utapata furaha pia

Mithali 14:30 "Moyo uliyo mzima ni uhai wa mwili bali husuda ni ubovu wa mifupa" wapo watu wamedhoofika afya na kuzeeka kabla ya muda wao sababu ya kushindwa tuu kusamehe

Mathayo 5:9 "Heri wapatanishi maana hao wataitwa wana wa Mungu" unaposamehe unajipatanisha na aliyekukosea na pia unajipatanisha na Mungu na kwa kufanya hivyo unapata sifa ya kuwa mwana wa Mungu

Kumbuka unakuwa unalipa jema kwa baya na hii ni baraka Luka 6:27 "Lakini nawaambia ninyi mnaosikia, wapendeni adui zenu, na watendeeni mema wale wanaowachukia ninyi"

Mwanamke Thamani!

1 comment:

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana