SUBIRA YAVUTA HERI - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Thursday, July 19, 2018

SUBIRA YAVUTA HERI






Moyo wa subira ni ule uwezo wa kuwa na uvumilivu, mpaka jambo fulani litakapotukia pasipo kukata tamaa wala kupoteza matumaini, moyo wa subira umejengwa juu ya uvumilivu na unyenyekevu

Kuna tofauti kubwa sana kati ya uvumilivu na unyenyekevu, uvumilivu ni hali ya kustahimili katika mazingira fulani pasipo kukata tamaa wala kurudi nyuma, unyenyekevu ni hali ya kuwa na moyo wa kujishusha na kutambua ya kwamba binadamu wenzako hawajakamilika na wana mapungufu

Siku tano zilizopita tulikuwa tunafundisha juu ya familia na kama haukusoma makala ya tano ya Uponyaji kwenye familia ⇉⇉⇉ UNAWEZA KUBOFYA HAPA

Mtu ambaye ananyenyekea ndiye anayeinuliwa Yak 4:10 "Jidhilini mbele za Bwana naye atawakuza, neno Jidhilini lina maana sawa na nyenyekea, hivyo mtu anayenyenyekea huuliza maswali 

Kunyenyekea siyo kuwa mnyonge, kuwa mnyonge ni kuwa mtumwa, naam ni kuvumilia visivyovumilika lakini mnyenyekevu siyo mtu mnyonge bali ni mtu anayeuliza pale inapobidi ili kupata mafafanuzi zaidi

Biblia inamtaja Musa kama binadamu aliyekuwa mnyenyekevu na mpole  kuliko wanadamu wote waliokuwa juu ya uso wa nchi Hesabu 12:3, lakini ukisoma zaidi historia ya uongozi wa Musa utagundua kuna baadhi ya sehemu alikuwa pia akimwambia Mungu maneno magumu

Kuna sehemu alimwambia kwamba hajawazaa Waisraeli Hesabu 11:12 "Je mimi niliyewatungisha mimba watu hawa wote je! Ni mimi niliyewazaa, hata ikawa wewe kuniambia, Haya, wachukukue kifuani mwako,....." ndio maana nikasema kunyenyekea siyo kuwa mnyonge

Mnyenyekevu anauliza maswali na ana muda wa kujadiliana na Mungu na hata na wanadamu wenzake lakini mnyonge hana nafasi hiyo ndio maana unapaswa kukataa kuwa mnyonge kwa moyo na mwili wako wote

Watu wengi wakishuhudiwa kitu fulani kitatukia hufikiri kesho yake ndio kitatukia au wiki ijayo huwa na haraka na pupa katika kila suala lao

Ni bora kwenda taratibu kuliko kuharakia lile ambalo Mungu amekuandalia, maana pupa huwaingiza watu kwenye majaribu na changamoto ambazo hawakupaswa kuingia

Yesu alijua kabisa tangu amezaliwa kwamba amekuja kuhubiri Injili, wakati fulani kwenye Biblia akiwa na miaka 12 alikwenda hekaluni na kuongea maneno ya hekima yaliyowaacha viongozi wa dini na mshangao

Japokuwa alifahamu kusudi lake hakukurupuka na kulianza kabla ya wakati bali alikuwa na subira hata alipofikisha miaka 30 ndio akaanza kuihubiri Injili

Hatupaswi kuhairisha mambo lakini kabla ya kuanza mchakato wa kile unachotaka kufanya mshirikishe Mungu suala lako

Watu wengi hurukia vitu pasipo kumshirikisha Mungu na mara nyingi hufika katikati na kugundua walikosea tangu awali

Wengine kwa mioyo migumu hukataa kugeuza gari (kubadili uelekeo) wachache huwa tayari kuanza tena upya 

Mtu mwenye subira pale anapopata ufunuo na anajua huu umetoka kwa Mungu huwa na uhakika kwamba utatimia

Moyo wenye subira huonesha ukomavu wa kiimani, ndoa yenye subira ni ile inayomtumaini Mungu na kuamini neno lake hata kama kuna miaka 5 imepita pasipo kupata mtoto

Wapo watu ambao wameoneshwa namna watakavyokuwa wakuu na wanafanya makosa kwa kutumia akili zao kujishawishi kwamba itawachukua muda mrefu sana kufikia ukuu wao

Leo nataka kuwakumbusha hata kama itakuchukua miaka 40 kutimiza ulichooneshwa haupaswi kuogopa wala kukosa subira

Hii ni kwa sababu muda utapita tuu uamini au usiamini kwa sababu hivyo ndivyo ilivyo jambo la msingi ni kuwa na mahusiano mazuri na Mungu

Wote tunamkumbuka Yusufu akiwa kijana kabisa Mungu alimuonesha katika ndoto namna atakavyokuja kuwa mkuu na kuwatawala ndugu zake

Baada ya kuelezea ndoto hii ndugu zake walijawa na wivu na kupanga njama za kumuuwa, lakini baadae nduguye mmoja aliwashawishi wamuuze utumwani

Jaribu kufikiri Mungu kakuonesha ukuu ulioko mbele yako na baada ya kuutamka umegeuka kuwa mtumwa, baada ya hapo tunakumbuka aliswekwa jela

Na kule alitabiria maakida wa Farao ndoto mara ya kwanza na Mwanzo 40:14 baada ya kuwatafsiria aliomba ombi " Unikumbuke , unifanyie fadhili, ukanitaje kwa Farao na kunitoa katika nyumba hii"

Tizama kilichotokea, maakida hawa yalitukia mema kama alivyowatafsiria na walipata nyadhifa zao lakini kamwe hawakumkumbuka Yusufu

Kama nilivyokwisha kusema mtu anayemwamini Mungu ana subira hajali itamchukua muda gani kufanikisha kile ambacho Mungu kamuambia

Wengi wetu tungekata tamaa kwa sababu tungesema tumemtumikia Mungu vya kutosha, tumetabiri ndoto na zimetukia na bado tuu tunakaa gerezani

Tungehoji maswali kama huyu Mungu yuko wapi? Je ndoto aliyonionesha ilikuwa ya kweli au siyo? Kwa nini ananiacha nateseka kiasi hiki natenda mema lakini nalipwa mabaya

Lakini siyo Yusufu alionesha subira huku akimtumaini Mungu kwamba atamfanikisha hata kama haikuwa wakati ule

Wakati ulifika Farao akaota ndoto na walipotafuta mtu kote wa kutafsiri ndoto ile hakupatikana isipokuwa mtu mmoja mwenye subira na aliyemwamini Mungu

Kumtumikia Mungu kunalipa hapa Yusufu alichangamkia tenda chap chap na kutokea mlango huo alikuwa waziri mkuu wa Misri umeona sasa?

Angekosa subira na kumlaumu Mungu kwa wale maakida wa mwanzo kutomkumbuka angepoteza hii nafasi ya ukuu na heshima

Ukiwa kama Mkristo subira ni lazima siyo ombi, haupaswi kukurupukia mambo, Mungu amekupangia mambo mema kuliko unavyofikiri kwa akili yako ya kibinadamu

Kumbuka Yusufu aliyekuwa anadharaulika na kuonekana hafai Mungu alifanya suala lake kuwa la tofauti, wewe unawasiwasi wa nini?

Waache wakucheke, wakudharau, waambiane mabaya yako lakini kama yanakupata yote haya ukimtumikia Mungu wa kweli na kutokea moyoni....

Yafaa nini kuhangaikia dunia na mambo yake yote?, Kuna siku watauona wema wa Mungu maishani mwako hapo ndipo watajua subira, tumaini, upendo na imani yako havikuwa vya bure

Mwanamke Thamani "Wewe umewazidi wote"

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana