MUNGU ANAYEJIFICHA- SEHEMU YA TATU - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Sunday, September 30, 2018

MUNGU ANAYEJIFICHA- SEHEMU YA TATU


Bwana Yesu asifiwe! Ninakusalimu sana katika Jina lipitalo majina yote mbinguni hata duniani, lenye mamlaka na uweza, ninatumaini umeamka salama na unaendelea vyema na kazi zako, leo ni siku njema sana mwanzo wa juma na kila juma lina baraka zake, ni maombi yangu ukutane na baraka zako zote Mungu alizokuandalia juma hili katika Jina la Yesu Kristo

Tunaendelea na kichwa cha somo letu Mungu anayejificha, tuliona katika masomo mawili yaliyopita Mungu kuna nyakati huuficha uso wake kwetu kwa sababu maalumu, leo kipekee katika somo hili tutaangalia ni nini cha kufanya Mungu anapojificha na madhara ya Mungu kujificha kwa muda mrefu

Tulipoishia....

Unamtumaini Bwana kwa nini? Jibu tunalipata mstari unaofuata 4 "Neno moja nimelitaka kwa BWANA, Nalo ndilo nitakalofuata, nikae nyumbani mwa BWANA siku zote za maisha yangu, Niutazame uzuri wa BWANA na kutafakari hekaluni mwake hii itapelekea Zaburi 27:5 "Maana atanisitiri bandani mwake siku ya mabaya, atanisitiri katika sitara ya hema yake, Na kuniinua juu ya mwamba

Kama hukupata nafasi kujifunza nasi somo lililopita bado unaweza kujifunza leo pamoja nasi kwa ⇒⇒⇒Kubofya hapa kujifunza

Tunaendelea....

Tumeona katika somo lililopita Mungu hujificha na hili halina mjadala hata ukisoma Isaya 45:15 "Hakika wewe u Mungu ujifichae nafsi yako, Ee Mungu wa Israeli, Mwokozi" hii inathibitisha kwamba upo wakati ambao Mungu hujificha kwetu kwa sababu maalumu

Mara nyingi watu ambao wameokoka au wapo kwenye wokovu kwa muda lakini hawalijui jambo hili linapowatokea hufadhaika na kuona kwamba Mungu amewatupa au hawasikii lakini sio kweli, katika wokovu kuna mitihani yake ambayo ili upande kiwango cha imani ni lazima ufaulu ndipo Mungu anakupa nafasi nzuri zaidi Mathayo 24:13 "Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka"

Hivyo unapoona Mungu kaficha uso wake jua ni kwa kitambo na kuna sehemu anataka kukupeleka jambo la kufanya ni kuendelea kukomaa naye na kumngojea mpaka atakapokuletea tena kwa wakati mwingine Nabii Isaya alilielezea vyema sana jambo hili Isaya 8:17 "Nami nitamngojea BWANA, awafichae uso wake nyumba ya Yakobo, nami nitamtazamia

Mungu alivyo wa ajabu anaweza kufichia uso wake nchi nzima kwa sababu ya uovu kama vile alivyofanya kwa nyumba ya Yakobo, ndiyo maana unaambiwa wokovu ni suala binafsi siyo la taasisi unaamua mwenyewe kumtafuta Mungu, usisubiri ushauriwe au uambiwe na mtu Nabii Isaya hajasema tutamngojea BWANA, bali nitamngojea BWANA, yeye peke yake

Yapo madhara ya Mungu kuuficha uso wake kwetu kwa muda mrefu, kama tulivyoona katika masomo yaliyopita Mungu hujificha kwa dakika moja inapozidi dakika moja madhara hutokea, lakini nataka ufahamu kwamba muda wa Mungu kujificha zaidi ni wewe unaamua, kama usiposhikamana nae kwa nguvu zaidi ni rahisi kukengeuka

Hii ndiyo sababu kubwa unaweza kushangaa watu waliokuwapo kwenye wokovu kwa muda mrefu wamerudi nyuma Mtume Paulo alilielezea hili vyema zaidi Waebrania 6:4-6 "Kwa maana hao waliokwisha kupewa nuru, na kuonja kipawa cha mbinguni na kufanywa washirika wa Roho Mtakatifu, Na kuonja neno zuri la Mungu, na nguvu za wakati ujao, Wakaanguka baada ya hayo, haiwezekani kuwafanya upya tena hata wakatubu; kwa kumsulubisha Mwana wa Mungu mara ya pili kwa nafsi zao, na kumtweza hadharani kwa dhahiri

Mungu anapokuficha uso wake jambo la kwanza ni kwamba utaangukia shimoni Zaburi 143:7 "Ee BWANA, unijibu hima, roho yangu imelegea; usinifiche uso wako, Nisifanane nao washukao shimoni, hivyo watu ambao wanatumbukia katika matatizo ni Mungu kawaficha uso wake

Kufadhaika, kukosa raha na kuumia moyoni na hata kifo husababishwa na Mungu kutuficha uso wake, Mungu hakuumba watu ili wateseke wala wapate matatizo bali wafurahie na kumtumikia katika roho na kweli, hivyo kifo chochote kile kinachotokea nje ya muda au kukosa furaha hakutokani na Mungu Zaburi 104:29 "Wewe wauficha uso wako, Wao wafadhaika; Waiondoa pumzi yao, wanakufa, Na kuyarudia mavumbi yao

Mungu akikuficha uso wake unakuwa mtu asie na makao duniani, watu wote wanaotangatanga na maisha yanaonekana kupishana nao ni kwa sababu Mungu amewaficha uso wake Mwanzo 4:14 " Tazama, umenifukuza leo katika uso wa ardhi, nitasitirika mbali na uso wako, nami nitakuwa mtoro na mtu asiye na makao duniani; hata itakuwa kila anionaye ataniuwa"

Itaendelea tena....

Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote
Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;

SALA YA TOBA

Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani

Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 

Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana

Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa
whatsup nambari 0715113636

2 comments:

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana