MUNGU ANAYEJIFICHA- SEHEMU YA PILI - MWANAMKE THAMANI

TV Online Channel

Friday, September 28, 2018

MUNGU ANAYEJIFICHA- SEHEMU YA PILI


Ninakusalimu katika Jina la Bwana wetu Yesu Kristo mwokozi wetu, leo tena ni siku nzuri ambayo Bwana ameifanya ili tumsifu na kumtukuza, ninatumaini unaendelea vema na kazi zako na mkono wa Bwana haujakupungukia katika kila hatua unayoichukua

Leo tutaendelea sehemu ya pili ya somo la jana Mungu anayejificha jana tuliona sababu moja ya kwa nini Mungu anajificha ambayo ni uovu, leo tena tunaendelea kama hukupata muda wa kujifunza nasi jana unaweza ⇒⇒⇒bofya hapa kujifunza nasi

Tulipoishia...

Katika lugha ya kiroho "kifungo" siyo lazima iwe ni kwenda jela, Hapana! kifungo ni jambo lolote lile ambalo linakuzuia kupiga hatua katika maisha yako, twajua watu wote walioko magerezani hawawezi kufanya biashara au shughuli zao za kawaida, hivyo kifungo inaweza kuwa ni magonjwa, umasikini, kukosa uzao na hata changamoto za ndoa

Tunaendelea...
Kama wewe ni msomaji mzuri wa Neno la Mungu utagundua kitu kimoja kwenye zaburi, mwandishi wa zaburi Mfalme Daudi kuna siri alikuwa ameigundua juu ya Mungu ndio maana alikuwa anapenda sana kutumia maneno haya inuka, unione, usijifiche, nimekutumainia, usinisahau, unilinde, ukiyachunguza vizuri maneno yote haya yanamuomba Mungu asijifiche kwake hata dakika moja

Mfalme Daudi alikuwa simba wa vita, hakuna Mfalme Israeli aliyewahi kupigana vita vingi kama yeye na hakuwahi kushindwa vita hata siku moja, kwa sababu  Mungu aliuona moyo wake na kabla ya kwenda kwenye vita alikuwa anataka Mungu amuhakikishie kama atashinda au hatashinda

Mungu anajificha na watu hawaoni uso wake kwa sababu ya ukaidi na kufuata njia zao wenyewe, Mungu alituumba ili tuwe na mahusiano naye katika kila kitu, anataka tudumishe mapenzi naye, isitoshe ukaribu wako na Mungu ni mkubwa kuliko hata wa mume au mke wako, unapoamua kufuata njia zako mwenyewe ina maana unamwambia Mungu wewe hujui kama mimi ninavyojua hivyo niache, katika hali kama hii hata kama mimi ningekuwa Mungu ningejificha nikuone utaishia wapi

Mungu alikuwa anampenda Mfalme Daudi kwa sababu alilishika neno lake, alimuuliza Mungu jambo lolote kabla ya kulifanya, kanisa ambalo ni mimi na wewe ni wake za Mungu kwa namna nyingine ni mabikira wake, anashangazwa kwa nini wake zake wanafanya maamuzi bila kumshirikisha, kumbuka Mungu ana mpango maalumu kwa ajili yako anasubiri tuu umwulize akupe wote

Isaya 57:17 "Kwa sababu ya uovu wa kutamani kwake niliona hasira, nikampiga; nilificha uso wangu, nikaona ghadhabu; naye akaendelea kwa ukaidi, kuifuata njia ya moyo wake mwenyewe

Usifikiri kwamba Mungu anauficha uso wake kwako kwa mwaka mzima hapana ni kwa dakika moja tuu, lakini hakuna rangi utaacha ona ila tunapaswa kukumbuka siku moja kwa Mungu ni sawa na miaka elfu moja kwa binadamu hivyo kuna mahesabu ya kupiga hapo Isaya 57:8 "Kwa ghadhabu ifurikayo nilikuficha uso wangu dakika moja;....."

Sababu zaidi za Mungu kuficha uso wake kwetu ni pamoja na hizi...

Mungu aweza kujificha kwako ili kuimarisha shauku yako kwake umtafute zaidi, Yer 29:13 "Nanyi mtanitafuta na kuniona mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote" Mungu anataka umtafute kwa moyo wako wote na siyo kwa mdomo wako tuu anataka akikaa mbinguni akitizama moyoni mwako anaona jina lake pekee

Hata hivyo Mungu anatuambia hivi katika Zaburi 27:8 "Uliposema, "Nitafuteni uso wangu" Moyo wangu umekuambia, BWANA, uso wako nitautafuta, hivyo ni sharti kumtafuta Mungu kuwe ni kutokea moyoni 

Mungu anapojificha inaweza kuwa ni kwa sababu ya kukutengeneza kwa ajili ya sehemu nyingine nzuri zaidi, tunamkumbuka Ayubu namna ambavyo Mungu alimruhusu adui amjaribu, lakini hata baada ya majaribu bado Ayubu aliendelea kumlilia Mungu na mwishowe Mungu alimuimarisha katika imani na katika mafanikio, alipata utajiri mara mbili zaidi, hata hivyo uzao ulirudia kama wa awali ila wa sasa ulikuwa na mabinti walimbwende zaidi

Ayubu 42:12 "Basi hivyo BWANA akaubariki huo mwisho wa Ayubu zaidi ya mwanzo wake; naye alikuwa na kondoo elfu kumi na nne, na ngamia elfu sita, na jozi za n'gombe elfu moja, na punda wake elfu moja, Mstari 15  "Katika nchi hiyo yote hawakuwapo wanawake waliokuwako wazuri kama hao wana wa Ayubu

Mungu anapojificha inaweza kuwa ni kwa sababu anataka akuandae kwa ajili ya changamoto inayoweza kutokea, hivyo anataka uendelee kuwa nyumbani mwake ili uweze kuishinda Zaburi 27:3 "Jeshi lijapojipanga kupigana nami, moyo wangu hautaogopa, Vita vijapotokea, hata hivyo nitamtumaini BWANA

Unamtumaini Bwana kwa nini? Jibu tunalipata mstari unaofuata 4 "Neno moja nimelitaka kwa BWANA, Nalo ndilo nitakalofuata, nikae nyumbani mwa BWANA siku zote za maisha yangu, Niutazame uzuri wa BWANA na kutafakari hekaluni mwake hii itapelekea Zaburi 27:5 "Maana atanisitiri bandani mwake siku ya mabaya, atanisitiri katika sitara ya hema yake, Na kuniinua juu ya mwamba

Itaendelea tena Mungu akubariki sana.......
Baba/kaka / mama/ dada/ Yesu Kristo anakuita tena leo anakuambia njoo uisikie sauti yangu nami nitakuponya na kukuondolea maangamizo yote
Kama amenibadilisha mimi na wengine wengi nina uhakika hata wewe anaweza kukubadilisha, haijalishi unapitia magumu gani muda huu lakini wakati wa uliokubalika ni sasa na ni kwa ajili ya maisha yako mwenyewe, kama unakubaliana nami fuata sala hii fupi ya toba sema;

SALA YA TOBA

Bwana Yesu ninakuja mbele zako mimi....................(taja jina lako) ninakiri kwamba nimekutenda dhambi na ninastahili kuhukumiwa


Lakini kwa sababu wewe ni Mungu mwenye rehema na neema naomba unisamehe, unioshe na kunisafisha kwa damu yako ya thamani uliyoimwaga pale msalabani

Ninaomba ufute jina langu kwenye kitabu cha hukumu na uliandike kwenye kitabu cha uzima, karibu Yesu ndani yangu ya kale yamepita na tazama yamekuwa mapya. Ahsante Yesu kwa kuniokoa Amen.


Hongera, kwa kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, huu ni mwanzo mpya wa maisha yako ndani ya Kristo Yesu 


Na kwa kuwa umetamka maneno hayo kwa imani wewe ni kiumbe kipya kumbuka unahitaji kujijenga kiroho zaidi tuna mafunzo maalumu kwa ajili yako wasiliana nasi kwa simu nambari/ Whatsup 0715113636 ili tuendelee kukuombea na kukushirikisha neno zaidi, Mungu akubariki sana

Kama unatamani kuwa mmoja wa wanachama wa Mwanamke Thamani (MT) na kujiunga nasi kuomba, kujifunza neno la Mungu kwa pamoja kama familia moja tunakukaribisha sana waweza kuwasiliana nasi kwa
whatsup nambari 0715113636

No comments:

Post a Comment

Unaweza kutoa ushauri au kuwasiliana nasi kwa mafunzo zaidi, karibu sana